Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema kamwe Tanzania haitaiomba radhi Rwanda, baada ya Rais Jakaya Kikwete kuishauri nchi hiyo kufanya mazungumzo na upinzani ili kumaliza vita katika eneo hilo la Maziwa Makuu.
Serikali ya Rwanda iliitaka Tanzania iombe radhi
kwa madai kuwa kauli ya Rais Kikwete ni kama tusi kwao na kwamba wao
hawawezi kukaa na kuzungumza wapinzani ambao ni wauaji.
“Kama Rwanda haitaki kufuata ushauri wa Rais Kikwete inatakiwa kuuacha na siyo kumtaka aombe radhi,” alisema.
Membe alitoa ufafanuzi huo bungeni jana wakati
akijibu hoja mbalimbali za wabunge katika mjadala wa makadirio ya
matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka
2013/2014.
Tamko hilo la Serikali limekuja ikiwa zimepita
takriban siku sita tangu Serikali ya Rwanda kutoa tamko la kupinga
ushauri huo uliotolewa na Rais Kikwete wakati akiwa katika sherehe za
maadhimisho ya miaka 50 ya Umoja wa Afrika (AU), uliofanyika mjini Addis
Ababa, Ethiopia.
Akijibu pendekezo hilo la Rais Kikwete, Waziri wa
Mambo ya Nje wa Rwanda, Louise Mushikiwabo alisema kuwa Rwanda haiko
tayari kufanya mazungumzo na watu ambao walishiriki kwenye mauaji ya
kimbari ya mwaka 1994, dhidi ya Watutsi na kwamba kufanya hivyo ni sawa
na kuhalalisha mauaji kwa wananchi wake.
“ Wale wote wanaodhani kuwa Rwanda itaanzisha
majadiliano na waasi wa FDLR nadhani kwa ukweli hawajui kile
wanachozungumza. Rwanda haiwezi kujadiliana na wauaji,” alisema waziri
huyo wakati akizungumza na Idhaa ya Kimataifa ya Radio Ufaransa.
Alisema kuwa wakati serikali ya Rwanda imefaulu
kuzika mienendo inayopalilia mauaji ya halaiki, lakini bahati mbaya
kumesalia makundi ya watu ambayo bado yanahubiri itikadi zinazokumbusha
uchungu na kutonesha kidonda kilicholeta maafa makubwa kwa wananchi.
“ Kumbe kuna wasemaji wengi wa kundi la FDLR.
Wengine wao wanaendelea kufungamana na itikadi za kundi hili. Rwanda
ilifaulu kutokomeza mauaji ya halaiki lakini hatukutokomeza itikadi za
kundi hili,” alisema waziri huyo.
Kauli ya waziri huyo imeungwa mkono na baadhi ya
wasomi pamoja na wanaharakati waliosema kuwa kuiomba Rwanda ianzishe
majadiliano na kundi hilo, wanapaswa kufikiri mara mbili.
Katika ufafanuzi wake Membe alimnukuu Waziri Mkuu
wa zamani wa Israel, Isaack Rabin kwamba mwaka 1995 aliwahi kutoa tamko
lililosema, ‘Tunajenga amani na tunajadiliana na maadui zetu na si
marafiki’.
Alisema kama Serikali ya Rwanda itakuwa imesikia
kauli hiyo inatakiwa kufanya mazungumzo ya amani na maadui, na wasingoje
kufanya mazungumzo ya amani na Tanzania, ambayo wana uhusiano mzuri na ni nchi rafiki kwa muda mrefu.
“Sijui kwa nini wanaliepuka suala hili. Israel na Palestina
wanazungumza, sasa wao ni nani mpaka wakatae kufanya mazungumzo? Sasa
watapigana mpaka lini wakati wameshindwa kutatua tatizo hilo kwa miaka
16?” alihoji Membe na kuongeza;
“Sijui kwa nini wanaona aibu kufanya mazungumzo na
upinzani. Ningependa serikali ya Rwanda ijue kuwa kwa tabia yetu tangu
uhuru tunatoa kipaumbele kwa mazungumzo ya amani.
Tumekwenda katika
kikundi cha M23 na tumemhimiza Rais Yoweri Museveni wa Uganda afanye
mazungumzo.”
No comments:
Post a Comment